Saturday, April 23, 2011

JK ADANGANYWA TENA SASA AMEPOTOSHWA ZAIDI YA MARA 12

WIKI chache baada ya Rais Jakaya Kikwete kutoa agizo akitaka uzio wa viwanja vya michezo Jangwani ubomolewe, imebainika kuwa agizo hilo limeshindwa kutekelezeka kwa sababu eneo hilo limeuzwa kwa mwekezaji ambaye ni raia wa China. Hivyo watendaji wa Halmashauri ya Ilala na Wizara ya Ardhi wanabanwa na masharti ya mkataba unaodaiwa kuingiwa baina yao na mwekezaji huyo. Imebainika kuwa Rais Kikwete alitoa agizo hilo Aprili 3 mwaka huu baada ya kupewa taarifa potofu na hivyo kutoa amri ambayo haitekelezeki kisheria.

Akiweka jiwe la msingi la upanuzi wa barabara ya New Bagamoyo, eneo la Mwenge-Tegeta, Rais Kikwete aliagiza uzio huo ubomolewe lakini hadi jana hakuna bomoabomoa yoyote iliyokuwa imefanywa katika eneo hilo. Wakati Waziri wa Ujenzi, John Magufuli, akipewa onyo na Rais Kikwete akitakiwa aache ubabe wa kubomoa maeneo ya watu, agizo hilo la Rais limekuwa ni kinyume na maagizo yake mwenyewe kwa waziri wake. Baada ya agizo hilo la Rais kuonekana halitekelezeki kisheria, hivyo jitihada za makusudi zinafanywa kujaribu kuvunja sheria ili kulinda heshima ya Rais.

Halmashauri ya Ilala na Wizara ya Ardhi katika siku za hivi karibuni zimekuwa zikitupiana mpira kuhusu nani hasa anayestahili kutekeleza agizo hilo la Rais, huku mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, Gabriel Fuime, akisema wameambiwa wasubiri kwanza. Chanzo chetu kutoka ndani ya halmashauri ya Ilala kilisema mkataba huo umempa mwekezaji huyo haki ya kujenga maghala mbalimbali ‘magodauni’, kwa makubaliano kwamba yangeinufaisha pia halmashauri hiyo.

Ilibainishwa zaidi kuwa mkataba huo uliingiwa kibinafsi na baadhi ya viongozi wa Ilala kutokana na tamaa ya fedha huku wakishindwa kuzingatia kuwa eneo hilo ni maalum kwa ajili ya michezo. “Unajua siasa inafika mahali watu wanajisahau....maana jambo hilo tumejitahidi kulizungumza kupitia vikao hata kuibuka mizozo ndani ya hivyo vikao lakini tunaishia kuzomewa,” alieleza. Alieleza kuwa mkataba huo ulipelekwa hadi katika semina ya madiwani iliyofanyika Januari 9 na 10 mwaka huu Landmark Hotel ili kupata baraka za madiwani, lakini baadhi waliupinga kwa kuwa haukufuata utaratibu. “Kwa kuwa viongozi wa Ilala wanajua fika kuwa kuna madiwani ambao wana midomo...walichokifanya ni kuwaweka karibu na inaonekana fedha imetumika ili kuwanyamazisha midomo,” kilifafanua.
Aidha, chanzo hicho kilieleza kuwa mikataba isiyokuwa na manufaa ndiyo inayosababisha halmashauri hiyo kuporomoka licha ya kuwa na vyanzo vingi vya mapato tofauti na wilaya ya Temeke.


Baadhi ya madiwani wamekuwa wakipiga kelele za mara kwa mara kuhusu uwanja huo wa michezo wa Jangwani lakini hakuna hatua zilizochukuliwa hadi sasa licha ya Rais Kikwete kutoa agizo lake. “Ni vigumu kwa watendaji wa halmashauri hiyo kuvunja uzio huo kwa sababu wao ndio walioshiriki kuingia mkataba huo mbovu. “Haya ndiyo mambo tunayopigia kelele kila wakati lakini hatusikilizwi maana halmashauri ina wataalam wa ardhi wa kutosha iweje wanashindwa kujua umuhimu wa viwanja vile?” kilihoji. Kilisisitiza kuwa kutokana na Rais Kikwete kuwa ndiye mhimili mkuu wa dola basi ana jukumu la kuhakikisha maagizo anayoyatoa yanatekelezwa ipasavyo.

Rais Kikwete ametakiwa kuingia na kusimamia agizo hilo binafsi kwa kwenda na kuvunja uzio huo mwenyewe kwani sio rahisi kwa walioingia mkataba kusimamia agizo hilo kutokana na kulinda maslahi yao. Hadi habari hii inaandikwa uzio wa mabati bado upo ndani ya viwanja hivyo huku wizara ikiitaka halmashauri ya Ilala ibomoe lakini majibu yanayotolewa na halmashauri hiyo ni kwamba wamezuiwa kufanya utekelezaji huo. Katika hotuba yake, Rais Kikwete aliiagiza wizara hiyo kubomoa mara moja mabati hayo kwa vile eneo hilo kwa jadi ni la viwanja vya kuchezea watoto na si la majengo.
“Na nyie watu wa ardhi, juzi nimepita Jangwani nikienda Morogoro na kuona mtu amezungushia mabati kwenye kiwanja cha kuchezea watoto. Kabomoeni wenyewe mabati yale,” alisema Rais Kikwete.

Hii si mara ya kwanza kudanganywa kwa Rais kwani ameshadanganywa zaidi ya mara 12 miongoni mwa mambo aliyodanganywa ni pamoja na ile ya kuzindua mradi wa Bwawa la Manchira lililoko wilayani Serengeti wakati tayari wananchi wamekwishafungua kesi Mahakama Kuu ya Mwanza wakidai fidia. Kesi hiyo iliyofunguliwa ni matokeo ya viongozi wa serikali wilayani humo kuhusika kuwalipa fidia watu wasiohusika na kuwaacha walengwa waliofanyiwa tathmini. Pia aliwahi kudanganywa kwamba daraja la Mkenda lililoko Ruvuma ambalo ni njia muhimu kuelekea Msumbiji, lilikuwa limekamilika.

Katika tukio jingine, Rais aliwahi kupewa taarifa zisizo sahihi kuhusu tuhuma za rushwa zilizokuwa zikimkababili Anatory Choya kisha akamteua kuwa mkuu wa wilaya, lakini siku siku chache baadaye akafunguliwa mashtaka na TAKUKURU.
Mwaka juzi, akiwa ziarani Mbeya msafara wa Rais ulishambuliwa kwa mawe na watu, lakini wasaidizi wake wakaja kutoa taarifa kwamba watu hao walikuwa ni wahuni na walikuwa wakimsubiri Rais kwa muda mrefu bila mafinikio. Hata hivyo, baadaye uchunguzi huru ulibainisha kwamba tukio hilo lilikuwa na mafungamano ya kisiasa na makovu ya mchakato wa uchaguzi ndani ya CCM kwa mwaka 2005.

Mlolongo huo mrefu wa upotoshaji taarifa kwa Rais uliibuka tena katika utoaji wa magari ya misaada ambapo badala ya kupewa mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Longido alipewa wa Ngorongoro. Tukio hilo lilimfanya mkuu huyo wa nchi kukasirika na kumzodoa mkurugenzi huyo, lakini baadaye ikabainika mkurugenzi huyo alikwenda kutokana na makosa ya maafisa wa Ikulu. Katika mlolongo huo, tukio kubwa kabisa ni Rais kutia saini kwa mbwembwe Sheria ya Gharama za Fedha za Uchaguzi ambayo ilichomekwa vipengele nje ya Bunge kitu ambacho ni kinyume cha sheria. Tukio hilo ambalo ni la uvunjifu wa Katiba, liliibuliwa na Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, ambaye awali, Mwanasheria Mkuu wa Serikali Jaji Fedrerick Werema, alikanusha.

Hata hivyo, baadaye sheria hiyo ilirudishwa bungeni na kukarabatiwa kwa mgongo wa mabadiliko ya sheria mbalimbali.
Mei mwaka jana, Rais alipewa taarifa za upotoshaji kuhusu mazungumzo ya Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) na serikali, kwa kuelezwa shirikisho hilo halikuhudhuria mkutano wa saa 4:00 asubuhi kama ilivyopangwa. Hata hivyo, TUCTA wakatoa ushahidi wa barua za mwaliko wa mkutano huo wa Aprili 22 mwaka jana, ambazo zilikuwa mbili moja ikionyesha walitakiwa kufika katika mazungumzo Hazina saa 4:00 asubuhi na nyingine saa 8:00 mchana. Katika kuonyesha upotoshaji kwa Rais, wasaidizi hao walimpa barua iliyokuwa ikionyesha walipaswa kukutana saa 4:00 asubuhi huku ile ya saa 8:00 wakawa wameificha. Rais akizungumza na wazee wa mkoa wa Dares Salaam aliwashambulia viongozi wa TUCTA hasa Naibu Katibu Mkuu, Nicolas Mgaya, akimwita mnafiki, mzandiki, na mchochezi.

TANZANIA DAIMA

No comments:

Post a Comment