Wednesday, February 09, 2011

Tushiriki kujenga nchi, si kusindikiza wengine

NI jambo linalotia moyo na hata kutia uhai mustakabali wa nchi. Kwamba; sehemu ya vijana nchini sasa wameanza kutambua nafasi yao katika ujenzi wa Taifa bora.
Tukio la vijana kuandaa kongamano la maadhimisho ya miaka 44 ya Azimio la Arusha, mwishoni mwa wiki hii, katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ni sehemu ya matukio yenye ishara nzuri katika kuijenga Tanzania kwa ajili ya Watanzania.
Kwa mujibu wa taarifa za waandaaji, ambao ni Chama cha Sauti ya Vijana Tanzania (SAVITA) katika Chuo Kikuu Dar es Salaam, wakati wa kongamano hilo kutafanyika tafakari-pacha.
Tafakari-pacha itakayohusu kwa upande mmoja; miaka 44 ya Azimio la Arusha ambalo liliweka misingi ya utu na maadili ya uongozi. Kwa upande mwingine katika tafakari hiyo ya kwanza, itatumbukizwa tafakari ya Katiba mpya.
Tunaungana na vijana hao katika tafakari hiyo ya mpigo, tukiamini inalenga kujenga Tanzania ya Watanzania. Tunaamini vijana hao hawatakuwa wazungumzaji tu wa Azimio la Arusha, bali watekelezaji kwa kadiri ya nafasi yao kijamii.
Kikubwa tunachotarajia ni washiriki wa kongamano kutoa maoni au hoja zenye kuonyesha upeo wao katika kujenga mustakabali wa nchi yao.
Hata hivyo, tahadhari yetu ni kwamba mawazo mapya ya vijana lazima yaenzi mawazo bora ya waasisi wa Taifa hili. Mawazo mapya ya vijana lazima yajitenge na unafiki.
Mawazo mapya ya vijana katika kongamano hilo yajitenge na maslahi yao kisiasa. Bila kutanguliza tofauti za itikadi zao kisiasa, wajadili na kufakari mustakabali wa nchi yao kwa faida ya vizazi  vingi vijavyo.

Watoe tafakari pevu ili kuthibitisha kuwa, ingawa wao ni vijana kwa umri, lakini upeo wao umevuka mipaka ya umri. Vijana watambue kuwa Tanzania itajengwa na Watanzania, nao ni sehemu ya hao Watanzania.
Tanzania ipewe nafasi ndani ya mioyo ya vijana. Watambue kuwa Tanzania kwanza, vyama vya siasa baadaye. Na kubwa zaidi, watambue kuwa wazalendo wa kweli hawana nchi ya mbadala, lazima wapiganie nchi yao, kwa maslahi yao na vizazi vijavyo.

Chanzo:Gazeti la RAIA MWEMA Februari 2, 2011 

No comments:

Post a Comment