TUHUMA za ufisadi katika uuzaji wa Benki ya NBC 97 Ltd zinatarajiwa kuanza kulipuliwa kwa nyaraka moja baada ya nyingine, wakati kesho mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia atakapoanza kutoa uthibitisho wa tuhuma zake dhidi ya benki hiyo iliyouzwa kwa Kampuni ya ABSA ya Afrika Kusini mwaka 2000.Mwaka 2003, Mbatia alilipua tuhuma nzito kuhusiana na mchakato wa uuzwaji wa benki hiyo akihoji uhalali wa kuuzwa kwa Sh 15 bilioni huku muda mfupi baadaye uchunguzi ukionyesha katika tawi moja pekee la Samora jijini Dar es Salaam, ilikuwa na deni la Sh 31 bilioni. Kwa mujibu wa wakili wa Mbatia, Dk Sengondo Mvungi kutoka Kampuni ya South Law Chamber, kesi hiyo ni ya kihistoria kwani inazungumzia mustakabali mzima wa nchi katika mambo ya ubinafsishaji. Tuhuma hizo za ufisadi katika mchakato wa uuzwaji wa NBC ziliwahi kumfanya Dk Harrison Mwakyembe, kujiuzulu ujumbe wa bodi kwa kile kilichodaiwa alikiuka taratibu kwa kutoa nje siri za vikao, kipindi ambacho joto la migomo na maandamano kupinga uuzwaji wa benki hiyo kwa ABSA ya makaburu wa Afrika Kusini, likiwa juu. Mwakyembe kwa sasa ni Mbunge wa Kyela na Naibu Waziri wa Ujenzi. Dk Mwakyembe baadaye katika taarifa yake ya ukurasa mmoja alisema:, "”Leo tarehe 18 Septemba 2003 nimewasilisha barua ya kujiuzulu kwenye Bodi ya Wakurugenzi ya NBC Ltd kwa Waziri wa Fedha Mheshimiwa Basil Mramba.” "Aidha, naamini kuwa kuondoka kwangu kwa hiari kutoka kwenye bodi hiyo kutatoa mwanya na fursa muhimu ya kwanza kwa Serikali kufanya mabadiliko ya msingi ya uwakilishi bora wa Serikali ndani ya NBC na hivyo kuwa chachu ya mabadiliko mengine ya msingi katika menejimenti ya benki hiyo.” “Naondoka kwenye bodi hiyo nikiwa na dhamira safi ya kwamba nimetimiza wajibu wangu wa kizalendo na Ahadi ya Nane ya Mwana-CCM isemayo: Nitasema kweli daima, fitina kwangu ni mwiko,” alisema Dk Mwakyembe, wakati sakata hilo likiwa tayari limekolezwa moto na Mbatia siku chache nyuma. Hata hivyo, ikiwa sasa ni karibu muongo mmoja tangu sakata hilo kuwa kimya huku mchakato wa kesi nao ukienda taratibu, mzimu huo umeibuka na Dk Mvungi akifafanua kuhusu Mbatia kuanza kutoa uthibitisho alisema:, "Ni kesi muhimu sana kwa taifa. Inebeba mambo mengi na mazito kuhusu mchakato wa ubinafsishaji..., wao (NBC), walilalamika kuitwa wezi na watu wenye utawala mbovu." .."Mbatia alihoji kama benki iliulizwa kwa Sh 15 bilioni iweje tawi moja tu la Samora katika kipindi cha muda mfupi liwe na deni la Sh 31 bilioni? Kwa hiyo inaonyesha thamani ya benki ilikuwa ni kubwa kuliko fedha ilizonunuliwa." Katika kesi hiyo pamoja na mambo mengine, Mbatia pia anadai kulipwa Sh 5bilioni baada ya kuitwa mbumbumbu na mtu asiyejua taratibu za ulali wa fedha na nyingine za kibenki, kitu kilichomchafua mbele ya jamii na watu anaowaongoza katika chama. "Sasa, baada ya Mbatia kutoa tuhuma hizo ndipo benki ikamwita kuwa ni mbumbumbu na mtu asiyejua mambo ya kibenki. Hivyo, kitendo hicho alikilalamikia akisema kimemchafua katika jamii kwani yeye ni kiongozi wa chama," alifafanua wakili huyo wa Mbatia. Kwa upande wake Mbatia, alisema amejiandaa vema kufyatua vielelezo kimoja baada ya kingine kuhusu tuhuma hizo na kusisitiza, "Nitatoa vielelezo kimoja baada ya kingine kuthibitisha niliyosema." Alifafanua kwamba, alichokizungumza kilikuwa na maslahi kwa taifa kwani Serikali ilikuwa na hisa asilimia 30 hivyo na kuongeza, "Ndiyo maana, tamko langu nilimpa Rais (wa awamu ya tatu), Benjamin Mkapa." "Septemba 16, 2003 nilitoa tamko na kulipeleka pia kwa Rais Mkapa (wakati huo) lakini wao wakatoa tamko lao wakiniita mimi mbumbumbu na mtu nisiyejua taratibu zozote za kibenki, sasa nitatoa nyaraka moja baada ya nyingine, " alitamba Mbatia. Uuzwaji hisa wa Benki ya NBC ni moja ya kitu kinachotajwa kama doa katika mchakato mzima wa ubinafsishaji, ukodishaji menejimenti na uuzaji hisa katika mashirika na makampuni ya Serikali chini ya Sera ya Ubinafsishaji iliyoratibiwa baada ya mageuzi ya kiuchumi kuanzia miaka ya 1990. SOURCE: MWANANCHI SUNDAY, 13 FEBRUARY 2011 |
Monday, February 14, 2011
TUHUMA UFISADI SH 31 BN ZA NBC KULIPULIWA
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment