Sunday, February 13, 2011

Mahojiano Ya Lowassa Na TBC; Tafsiri Yangu

Ndugu Zangu,
NDANI ya saa 24 baada ya tukio la Mapinduzi ya Umma kule Egypt, Edward Lowassa ,Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama ameonekana kwenye runinga akitoa tafsiri ya kilichotokea Egypt , nini cha kujifunza na kipi cha kufanya.
Lowassa alianza kwa kuwapongeza wanaharakati wa Misri. Akazungungumzia madhara ya viongozi kujilimbikizia mali, umuhimu wa viongozi kusoma alama za nyakati, athari za ubepari, umuhimu wa viongozi kusikiliza matatizo ya watu wao na mengineyo. Kimsingi, Edward Lowassa alizungumzia masuala yanayowahusu ‘ People On The Streets’- Watu wa mitaani, na kwa lugha inayoeleweka na watu wa mitaani.
Na kwa hakika, yanayotokea sasa ni Mapinduzi ya Umma wa Kijamaa barani Afrika. Kilio cha mamilioni ya Waafrika ni kilio cha kutaka uwepo wa Haki za Kijamii- Social Justice. Sera za Kibepari hazijali haki za kijamii. Ndio maana, Wajamaa wa Afrika tumeyapokea yalitokea Tunisia na Misri kwa mikono miwili. Ni fundisho kwa watawala wetu. Tusingependa vurugu za Tunisia na Egypt zifike kwetu, maana zina madhara makubwa ya kijamii na kiuchumi.
Hata hivyo, tunataka watawala wetu wasome sasa alama za nyakati. Waongoze mabadiliko ya amani ikiwamo mabadiliko makubwa ya Katiba ili tuepushe watu wetu kupoteza maisha na mali zao mara vurugu za kisiasa zitakapotokea. Na tusijidanganye, kuwa tuna amani, yetu ni amani ya vurumai.
Edward Lowassa ameonyesha ujasiri wa kujitokeza hadharani na kukiri , kuwa kuna mapungufu ya kimfumo, kwamba ubepari huu ndio umewafanya WaMisri waingie mitaani. Utajiri wa Mubarak unasemwa unaweza kuvuka utajiri wa Bill Gates. Wakati huo huo watu wa kawaida wa Misri wamekuwa wakiishi katika maisha magumu sana. Na Lowassa alionyesha hatari inayoweza kutokea kwetu . Amefikiri juu ya kipi kifanyike.
Mwanafalsafa Benjamin Disraeli anasema; “A good leader knows himself and the times”- Ndio maana pia ya kiongozi kuwa na uwezo wa kusoma alama za nyakati. Na kiongozi mzuri, hata katika nyakati ngumu, mara zote hujiweka katika nafasi ya ushindi.
Kwenye ulingo wa myeleka, hubaki katikati ya duara, atapigwa, ataanguka, atasimama. Atapigwa tena, ataanguka, atasimama. Hutokea kwa adui kuingiwa na mashaka na woga kutokana na ustahimilivu wa anayepigwa. Kwenye mchezo wa myeleka jitupe katikati upambane, kamwe usisimame kando ya duara, utaharakisha kazi ya adui kukutupa nje ya ulingo.
Na sifa moja ya mwanasiasa ni kuwa na uwezo wa kufanya yale ya kuwashangaza wengine, inahusu timing, inahusu wakati. Hata kabla ya Waziri wetu wa Mambo ya Nje hajaongea na wanahabari, Edward Lowassa , kwa nafasi yake ya uenyekiti wa kamati husika na mambo ya Ulinzi, Usalama na Nje ameongea na wanahabari. 
Na hakuongea kwa kukurupuka, Lowassa alionekana kuifanyia kazi taarifa yake. Si ndio, wanaomjua Edward Lowassa wanasema, kuwa jamaa ni workalcoholik, ana ulevi wa kuchapa kazi. Anafanya kazi kwa saa nyingi. Na kuna ujumbe aliutuma jana, kuwa Edward Lowassa amerudi. Baada ya kimya kirefu.
Lowassa huyu anaonekana kuwa bado ana nguvu na ushawishi ndani ya Bunge na Serikalini. Si tumeona, amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati nyeti bungeni bila kupingwa. Na kama ana dhamira ya kusimama, kugombea Urais 2015, basi, Edward Lowassa ana kazi moja kubwa inayomkabili ; kurudisha image yake ya zamani kwa umma, in principio, ya kama mwanzoni. Huu ni mtihani mgumu kwa Lowassa, akifaulu, 2015 hakamatiki.
Maana ni ukweli, kuwa Edward Lowassa wa sasa ni ’ libero’ uwanjani, hana wizara, lakini anaongoza Kamati nyeti na yenye nguvu kuliko zote bungeni. Lowassa huyu ni hatari kwa wapinzani wake katika kuelekea 2015 kuliko Edward Lowassa aliye Waziri Serikalini. Naam. Kuna burudani ya kisiasa inakuja.
Na kuna watakaoshika tama na kusema, kumbe, Edward Lowassa hajamalizwa kisiasa! Je, akina Mwakyembe hawakufahamu, kuwa simba humwui kwa risasi ya kumpapasa masikioni. Kama ni mchezo wa ngumi, basi, kwa mpinzani wa Lowassa, akubali, kuwa kummaliza Lowassa , awe tayari kucheza raundi zote 12.
Ndio, siasa inahusu pia sanaa ya mawasiliano, kwa mwanasiasa, kama huiwezi sanaa ya kuwasiliana na wananchi, basi, ni sawa na mtu anayejiita fundi mekanika , lakini hawezi kushika spana.
Tunayasema mabaya mengi ya Edward Lowassa, lakini, ni ukweli, kuwa Lowassa anaijua siasa na sanaa ya mawasiliano katika siasa. Katika mahojiano yale ya jana kwenye TBC, Lowassa aliwavuta anaowasiliana nao kwa kuanzia na mada husika na mahali alipochagua kufanyia mahojiano, palionekana kuwa ni nyumbani kwake, kule Dodoma. 
Kwa muonekano, Lowassa alionekana yuko simple. Alikaa kwenye kochi karibu kabisa na mwandishi anayemhoji. Na mwandishi naye alikaa kulia kwa Lowassa kwenye kochi linalofanana na la Lowassa.
Tulimwona Lowassa akiongea kwa utulivu na kwa mpangilio, Edward Lowassa ni mahiri wa rhetorik, sanaa ya kuongea. Katika dakika chache zile, Lowassa aliweza kuunganisha yaliyotokea Egypt na ya ’binadamu wadogo’ wa hapa kwetu na mahitaji yao, akiwa na maana ya mahitaji ya watu wadogo. Lowassa ni Mmasai, labda Umasaini kuna ng’ombe na binadamu tu!
Na hapa mtaona tofauti, miezi kadhaa iliyopita tuliona kupitia TBC, mahojiano ya Ben Mkapa na mwandishi Edson Sanga. Mkapa alikuwa akitoa maelezo kuhusu kazi yake kule Sudan, mahojiano yale hayakuwa na mvuto, ni kuanzia kwenye upangaji wa scene ya mahojiano. Mkapa alikaa kwenye kochi akiongea huku akiangalia chini na huku anayemhoji akiwa kushoto kwake amekaa kwenye kito tofauti na Mkapa na umbali wa mita kadhaa. Ni heri mwandishi angemhoji Mkapa kwa njia ya simu.
Naam, siasa ni burudani pia, tusubiri ya usiku wa leo, kwenye TBC1. ITV na kwingineko!
Maggid
Iringa,
Jumapili, Februari 13, 2011
 

No comments:

Post a Comment